Janga la mfumo mpya wa ubepari
Tunaanza uchambuzi wetu kuhusu ubepari jijini Nairobi tukiuliza: Je, kuna kitu kama mshahara mzuri siku hizi?
Mimi ni Gacheke. Mwaka wa 2017 nilikutana na rafiki yangu Antony Adoyo, ambaye kwa sasa ni mratibu wa jamii na wa utafiti unaoshirikisha wanajamii katika kamati ya uendeshaji wa vituo vya haki ya kijamii, inayoshirikisha sauti za wanaharakati wa jamii mabimbali. Wakati huo alikuwa anajitayarisha kutamatisha masomo yake katika chuo kikuu cha Nairobi, ambapo alikuwa mwanawafuzi wa masomo ya uchumi na fedha.
Adoyo alikuwa na ndoto ya kufanya kazi na Benki Kuu ya Kenya. Ndoto ambayo wanafunzi wenzake pia waliienzi. Walitumaini kuwa watapata kazi yenye mapato mazuri. Tulipokuwa tukijadiliana na Adoyo alinisihi nimsaidie kupata kazi kama mwanaharakati wa haki za binadamu kwenye mashirika makubwa. Nilishangaa kuwa msomi wa chuo kikuu nambari moja nchini Kenya angehitaji msaada wangu kupata kazi ya uharakati.
Adoyo alipohitimu mwaka wa elfu mbili na kumi na saba, alinialika pamoja na rafiki wengine kwenye karamu nyumbani kwao. Aliishi katika nyumba za kukodisha yenye vyumba viwili kule Dandora, mojawapo ya mitaa ya walalahoi ilioko karibu na Mathare. Baba yake aliongoza dua ya kumwomba Mwenyezi Mungu amsadie mwanawe kuleta matumaini na kuiondoa familia yake kwenye umaskini na taabu za Dandora. Tulisherehekea mlo wa chapati kwa nyama. Niliona jinsi familia hii iliyojikakamua kumsomesha mwanao ili aweze kuwaokoa kutoka umaskini.
Wanafunzi wengi hawatakua na uwezo wa kutoa familia zao katika umaskini ama kulipa mikopo ambayo wazazi wao walichukua mradi walipe karo ya chuo kikuu. Ni swala la haki ya kijamii kuwa wanafunzi wengi waliohitimu, wana shahada mbalimbali za uguuzi, kama za udaktari, uchumi, uhandisi na bioteknolojia. Shahada hizi zinawapa taswira ya waliopitia kwa miaka kuhitimu. Ukakamavu unaolipizwa na ukosefu wa kazi kwa miaka mitano baadaye na mingine. Wanaishi katika janga la ubepari kila siku.
Mwanafunzi mmoja wa masomo ya ujamaa aliilalamikia kuwa ameacha kuomba kazi akihofia kuwa huenda akapatana mchuuzi akitumia stakabadhi zake kufunga karanga. Alikuwa ametuma maombi yanayozidi mia na alishuku kuwa stakabadhi hizo zinatupwa kisha wachuuzi wanazitumia kufunga bidhaa vyao.