Ubaguzi wa vijana na mapambano ya kijamii
Vijana masikini wa jiji la Nairobi wanachukuliwa kama wahalifu kwa ajili ya vurugu za mfumo ambazo zinawanyima ajira, haki na uhuru.
Mimi ni Minoo. Nilizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Mukuru. Nimeshuhudia aina zote za ukatili wa polisi na ubaguzi wa vijana, pamoja na hali ya umaskini. Nimekutana na vijana kutoka mitaa ya matajiri na ilikuwa wazi kuwa hawajapambana na hali kama hii ya ubaguzi. Hii ni dhibitisho kuwa umaskini ni uhalifu. Mabepari na serikali wanaohalifisha umaskini ndio wanatusukuma kwenye umaskini ili tunapoomba chakula wanavuna jasho letu na kutulipa pesa kidogo zaidi.
Niliamua kuweka rasta kwenye nywele zangu, ila kama mkaazi wa Mukuru Kwa Njenga, nilikuwa na hofu nyingi sana. Niliona jinsi wenzangu walikamatwa wakiwa na nywele zao za rasta, waliaandikiwa mashtaka ya uwongo ya kupatikana na bangi au matendo mengine ya uhalifu. Hali huo mbovu ya vijana umewafanya watu katika jamii pia kuwaona vijana wenye nywele ndefu za rasta kama wahalifu au wanaotumia dawa za kulevya. Nilishuhudia rafiki yangu Kaparo akinyolewa na kipande cha mabati katika kituo cha polisi. Walidai kuwa alikuwa amepigana na mwana wa jasusi wa polisi. Binamu yangu pia na rafiki zake saba walikamatwa kwa madai ya kuwa na bhangi. Yeye na wenzake wane walinyolewa na mapolisi wakitumia wembe moja kati yao. Waliandikiwa mashataka ya uongo kuwa walikuwa wakipanga kuiba. Ilibidii wazazi wao kutoa hongo ili waachiliwe. Mwaka wa 2019, vijana nane wa kiume walipigwa risasi na polisi walipokuwa na mkutano wa kujadiliana kuhusu ukusanyaji wa takataka. Walikuwa na umri kati ya miaka 16 -24.
Nilisomea shule ya msingi ya Mukuru Kwa Njenga iliyokuwa karibu na nyumbani. Shule hiyo ilikuwa na uwanja mkubwa ambao vijana wengi walitumia kucheza mchezo wa kandanda. Lakini, usiku uwanja huo ulikuwa kichinjio. Kijana mmoja aliyekuwa muuzaji wa kitambo wa bangi alipigwa risasi muda wa saa mbili usiku. Polisi walidai kuwa alikuwa mhalifu na kumwekea kadi nyingi za simu na risasi bandia (bonoko).
Kila usiku, hata wakati mwingine mchana, mimi huskia milio ya risasi kutoka kwenye uwanja. Sikupitia ukatili mwingi sana kama mwanamke lakini nimewaona vijana wenzangu wa kiume wakiteseka kila siku. Wakati mwingine, baba yangu husema anamshukuru Mungu kwa kutopata mtoto wa kiume, kisa na maana hajui jinsi angeweza kumlinda dhidi ya ukatili huu unaofanyika katika mitaa ya walalahoi.
Ni hatari kuwa na mavazi za bei ghali kwani inahatarisha maisha yako. Unaweza kushtakiwa kwa wizi na kupigwa kikatili. Najua rafiki zangu ambao hawawezi kuvaa vizuri kwa sababu wamewahi kuwa jela kwa miaka mingi. Hata baada ya kubadili mienendo yao, maafisa wa polisi bado wana mazoea ya kuwanyanyasa, kuwapiga kikatili wakidai kuwa wanataka kujua walikoiba nguo hizo.
Nimenusurika katika huu mtaa nikiona jinsi serikali inavyopata pesa kwa kukandamiza maisha yetu. Serikali inaeneza woga kwa kutumia vurugu na jela. Tunahisi hali ya athari mahali ambapo tunapaita nyumbani. Nina marafiki wasio na hatia wanaozorota gerezani. Kosa lao ni kuwa maskini na kuishi katika mtaa duni. Hatukuchagua hali hii ya maisha.